Tuesday, 25 March 2014

WAADVENTISTA TUENDELEZE MOYO HUU WA HURUMA

Nawapongeza Waumini Sabato waliochangia damu


Askofu Malekana ametoa wito huo jana Makao Makuu ya Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dar es Salaam wakati kanisa hilo likiadhimisha Siku ya Vijana ya Matendo ya Huruma kwa Jamii kwa kuchangia damu Kituo cha Mkoa wa Dar es Salaam.
SHARE THIS STORY
0
Share


Dar es Salaam.
 Askofu Mkuu wa Kanisa la Adventista wa Sabato Jimbo la Mashariki Tanzania, Mark Malekana ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kuchangia damu ili kupunguza uhaba uliopo hapa nchini.
Askofu Malekana ametoa wito huo jana Makao Makuu ya Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dar es Salaam wakati kanisa hilo likiadhimisha Siku ya Vijana ya Matendo ya Huruma kwa Jamii kwa kuchangia damu Kituo cha Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kwa mujibu wa biblia, damu ni uhai. Damu hii tunayoitoa ni akiba kwa ajili yetu na wengine pia…ni vyema kufanya matendo ya huruma kwa wengine,” alisema Malekana.
Naye Ofisa Uhusiano wa Mradi wa Taifa wa Damu Salama, Rajab Mwenda alitoa wito hasa kwa vijana kujitokeza na kuchangia kwa kuwa wao ndiyo wenye afya nzuri ya kuweza kufanya hivyo.
“Tunadhamiria kukusanya chupa 150,000 mwaka huu baada ya kufikia malengo ya chupa 140, 000 mwaka jana. Changamoto kubwa ni mwitikio mdogo wa wanavyuo ambao ni muhimu sana katika kampeni hii,” alisema Mwenda.
Kampeni hiyo inalenga kukusanya zaidi ya chupa 3,000 katika vituo saba vya Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Tabora, Kilimanjaro, Zanzibar, Mtwara na Musoma. kituo cha Dar es Salaam pekee kinategemewa kuchangia chupa 800.
Mkurugenzi wa Huduma za Vijana wa kanisa hilo, Pasta Emmanuel Sumwa alisema kuwa uhamasishaji umeongezeka mwaka huu tofauti na mwaka uliopita.
“Vijana 1,600 walijitokeza katika jimbo zima mwaka jana, lakini mwaka huu tunatarajia idadi hiyo itaongezeka na damu nyingi zaidi itakusanywa,” aliongeza Sumwa.
Baraka Rabson, mmoja kati ya vijana waliochangia damu kutoka Kanisa la Ushindi lililopo Mikocheni B, aliwaasa vijana kujitoa kwa ajili ya jamii inayowazunguka ili kuonyesha uwajibikaji. “Ni mara yangu ya kwanza kuchangia damu. Nimefanya hivi ili kutoa mchango wangu kwa jamii yenye wagonjwa wasiojiweza vitandani. Wenzangu waniunge mkono,” aliasa Rabson. Takwimu zinaonyesha kuwa kuna upungufu wa damu chupa 400,000 kila mwaka kitaifa.

No comments:

Post a Comment